Karibu tujifunze habari ya mihuri SABA katika ufunuo sura ya 6
Tukisoma kitabu cha ufunuo sura ya tano, tunaona Mungu akiwa ameketi kwenye kiti chake cha enzi akiwa na kitabu katika mkono wake wa kuume, kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kikiwa kimetiwa mihuri saba. Na tunasoma hapakuonekana mtu yeyote mbinguni wala duniani aliyestahili kukifungua hicho kitabu wala kukitazama, kwani Ni kitabu kilichobeba siri zote za ukombozi wa mwanadamu,kuanzia mwanzo wa mambo yote hadi mwisho wake, jambo lililomfanya hata Yohana alie machozi kwa kuwa hapakuona mtu yeyote aliyestahili kukifungua wala kukitazama. Lakini mmoja tu aliyeonekana amestahili kukifungua hicho kitabu, naye ni BWANA wetu YESU KRISTO. (soma ufunuo sura ya tano yote.) utaona habari hiyo.
Lakini tukiendelea ile sura ya 6 tunaona Bwana Yesu akivunja mihuri ya kile kitabu. Kumbuka kile kitabu sio kama hivi vitabu tunavyoviona leo, bali ni vitabu vya kuzunguka (scroll), na mihuri yake ni kama vifungo.
Na kila muhuri ulipofunguliwa ulikuwa unaambatana na tukio fulani, moja baada ya lingine, mpaka mihuri yote 7 imalizike ndipo kitabu kifunguliwe. Ni vema kama hujafahamu bado juu ya NYAKATI 7 ZA KANISA (ufunuo 2&3), ukasome kwasababu mihuri hii inaendana sana na zile nyakati SABA za kabisa.
MUHURI WA KWANZA:
Ufunuo 6:1-2, “Kisha nikaona napo Mwana kondoo alipofungua moja ya zile muhuri saba, nikasikia mmoja wa wale wenye uhai wanne akisema, kama kwa sauti ya ngurumo, Njoo! nikaona na tazama, farasi mweupe na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, ali akishinda tena apate kushinda.”
Tunaona hapo kuna wale wenye uhai wanne na wale farasi wanne.Wale wenye uhai wanne walioonyeshwa katika sura hii, wanaashiria nguvu ya Mungu iliyoachiwa kwa watu wake, kupambana na uovu na njama za yule adui.Mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba, na wa pili alikuwa mfano wa ndama na wa tatu kama mwanadamu, na wanne kama tai arukaye.(Ufunuo 4:6-8). Vivyo hivyo na kwa wale farasi: farasi wa kwanza alikuwa ni mweupe, wa pili mwekundu, watatu ni mweusi na wanne ni wa rangi ya kijivujivu. Embu tuangalie ufunuo wa mambo haya kwa ufupi.
Kwahiyo muhuri wa kwanza ulipofunguliwa, yule mwenye uhai wa kwanza aliposema njoo! akatoka farasi mweupe, na aliyempanda juu yake ana uta (upinde wa mshale). Huyo farasi mweupe na aliyempanda ni roho ya mpinga Kristo ikianza kutembea katika kanisa la Mungu kwenye kanisa la kwanza Kabisa (EFESO) ,Lilidumu kwa kipindi cha kati ya AD 53- AD 170.
Mtume Paulo akiwa kama mjumbe wa kanisa hilo alisema hivi..2thesalonike 2:3 ” Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yeyote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu: akafunuliwa yule mwana wa kuasi, mwana wa uharibifu.” kwahiyo hapo tunaona kuwa mwisho wa yote usingefika kabla ya ule uharibifu( ukengeufu) kuja kwanza na kuingia katika kanisa. Na huo ukengeufu ndio ulipoanza na huyo farasi mweupe, kumbuka rangi nyeupe inaashiria usafi hivyo shetani alikuwa anajigeuza kama malaika wa nurukatikati ya kanisa lakini kwa ndani alikuwa ni mbwa mwitu mkali.(2 Wakoritho 11:13-15)
Hii roho ya shetani ilianza kuingia katika kanisa la kwanza baada ya mitume kuondoka hapa Paulo anasema matendo 20:29 ” najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.” 1Yohana 2:18 aliongezea kusema ” watoto ni wakati wa mwisho na kama vile mlivyosikia ya kwamba mpinga kristo yuaja, hata sasa wapinga kristo wengi wamekwisha kuwapo. kwasababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wakwetu wangalikaa pamoja nasi.Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu.”
Kwa hiyo hapa tunaona mitume walilionya kanisa lililokuwa kipindi kile juu ya mafundisho ya uwongo ambayo hayakuhubiriwa na mitume. Hivyo yule farasi mweupe ni roho ya mpinga kristo ikitembea katika kanisa la kwanza, na alionekana mweupe na aliyempanda ameshika uta (upinde) lakini hana mshale, kuashiria kutokuwa na madhara yoyote (yaani kuhusisha mauaji ya watakatifu) . roho hii ilanza kuingia kama mafundisho ya uwongo lakini Mungu aliachia Roho ya kuishinda iliyofananishwa na yule mwenye uhai wa kwanza ambaye ni mfano wa SIMBA aliyesema Njoo!. Tabia ya simba ni mnyama asiyeogopa, mwenye ujasiri hivyo wakristo wa kipindi kile waliweza kuishinda ile roho ya mpinga kristo kwa ujasiri wa neno la Mungu.
Kumbuka Nyakati hii ya mpanda farasi wa kwanza ilidumu kati ya kipindi cha 53AD-170AD. katika kanisa la kwanza ambalo ni Efeso.
Kristo alitoa pia angalizo kwa kanisa hili tunasoma katika kitabu cha ufunuo 2:2″ nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio ukawaona kuwa ni waongo……lakini unalo neno hili, ya kwamba wayachukia matendo ya wanikolai ambayo na mimi nayachukia.”.
MUHURI WA PILI:
Ufunuo 6:3-4 ” Na alipoifungua muhuri ya pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema Njoo!. akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyeimpanda alipewa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa.”
Hapa katika muhuri huu tunaona shetani (roho ya mpinga kristo), baada ya kuona kwamba ameshindwa kuwazuia wakristo wa kweli kumwabudu Mungu katika Roho na kweli wakisimamia neno wakiongozwa na ile nguvu ya Mungu kwa mfano wa simba ambayo ndiyo ile Roho ya Mungu aliyoiachia kwa watu wake kumshinda shetani,
Hivyo shetani akaamua kubadilisha mbinu zake za kuwashambulia wakristo, kwa kubadilika kutoka farasi mweupe kwenda kuwa farasi MWEKUNDU, na tunaona aliyempanda ni yule yule aliyekuwa anamwendesha yule farasi wa kwanza. Tunasoma kuwa alipewa mamlaka ya kuiondoa amani na upanga mkubwa mkononi mwake, kuashiria kuleta dhiki za mauaji kwa wale watu wanaomwamini Mungu na kuzishika amri zake, Kumbuka shetani huwa hafanyi vita na watu wote bali na watakatifu wa Mungu wanaolishika NENO lake.
Hii roho ya uovu(mpinga kristo) ilianza kama mafundisho yasiyohusisha mauaji, (ndiyo yale matendo ya wanikolai), baada ya kudumu muda mrefu yakatengeneza DINI, Na hii dini kumbuka ilianzia Roma kwasababu wakati ule RUMI ndio ilikuwa inatawala dunia, Wakati huo kulitokea makundi mawili, kundi lilishikilia mafundisho ya mitume tu! na lile lilichukua mafundisho yaliyochanganyikana na uongo. Ikapelekea kutokea mizozano kati ya haya makundi mawili, hivyo Rumi wakaunda dini moja chini ya mtawala(costantine), inayoitwa UNIVERSAL(CATHOLIC) CHURCH yaani DINI YA ULIMWENGU MZIMA. Hapo ndipo upagani wa kirumi ulipochanganyikana na Ukristo. Na ilipitishwa sheria yoyote atakayeonekana anaenda kinyume na DINI hiyo sheria ilikuwa ni moja tu! KIFO!!
Katika utawala wa Roma, Historia inaonyesha hadi kufikia kipindi cha matengenezo ya kanisa utawala wa Rumi chini ya kanisa katoliki ulifanikiwa kuwauwa wakristo zaidi ya milioni 68, kwa dhumuni la kuimarisha itikadi za dini yao. kwa mtu yeyote kuwa na imani nyingine nje ya dini ya kikatoliki adhabu ilikuwa ni kifo. Wakristo na wayahudi wengi waliuawa kwa kusimamia imani yao. damu nyingi za watakatifu zilimwagika.
Huu ndio ule upanga wa yule FARASI MWEKUNDU, alikuwa na kazi moja kuondoa amani katikati ya watakatifu. Na wakati huu wa farasi mwekundu ulitembea katika makanisa mawili yaani SMIRNA na PERGAMO. kati ya mwaka 170 AD -606 AD.
lakini pamoja na hayo Mungu alijua namna gani ya kuwashindia watueule wake hivyo aliachia Roho ya kuweza kuikabili hiyo nguvu ya mpinga kristo nayo ni nguvu iliyofananishwa na NDAMA (yaani YULE MWENYE UHAI WA PILI aliyesema njoo!), Ndama ni mnyenyekevu sana yupo tayari kwenda kuchinjwa na siku zote anaandaliwa kwa ajili ya kutolewa sadaka, hivyo wakristo wengi kwa kutaka wenyewe walijitoa maisha yao kwenda kuuawa kwa ajili ya imani yao bila kuogopa kwani Mungu ndiye aliyeachia hiyo Roho ya WEPESI juu yao, Kama vile tu BWANA wetu alivyokuwa mnyenyekevu akatii mpaka mauti ya msalaba, walichinjwa, walisulibiwa, waliliwa na simba, waliburutwa lakini kwa jinsi walivyozidi kuwauwa ndivyo walivyozidi kujitoa nafsi zao ziwe dhabihu .
warumi 8:36 ” …..kwa ajili yako tunauwa mchana kutwa, tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa” kipindi cha huyu farasi mwekundu kilidumu mpaka mwishoni mwa kanisa la pili.
MUHURI WA TATU:
Ufunuo 6:5 “na alipoifungua muhuri ya tatu,nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! nikaona, na tazama, FARASI MWEUSI, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wa nne, ikisema, kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai.”
Sasa baada ya shetani kuona anawaua wakristo na bado wanaendelea kukubali kwenda kuuawa kwa kuishikilia imani yao iliyoanzishwa na mitume na si vinginevyo wakipinga mafundisho ya dini ya uongo(yaani ya kikatoliki), akaamua kubadili mbinu ya kulivamia kanisa la Mungu kwa namna nyingine kwa kubadilisha rangi kutoka kuwa farasi mwekundu kwenda kuwa farasi mweusi.
Hichi ni kipindi kinachojulikana na wanahistoria wengi kama kipindi cha giza (dark age) kilidumu kwa zaidi ya miaka 1000 kuanzia karne ya 5 mpaka karne ya 16. Ni kipindi ambacho utawala wa kipapa chini ya dini ya kikatoliki ,ulianza kuuza kile wanachokiita neno la Mungu kwamfano mtu akitaka kuoa au kuolewa ni lazima atoe fedha, ibada za kuwaombea wafu (ambazo ni kinyume na neno la Mungu) ni lazima utozwe pesa, kushiriki meza ya Bwana ni lazima utozwe pesa, ukitaka kusamehewa dhambi unapaswa kutoa pesa, ukitaka kuombewa kama unaumwa ni lazima utoe pesa n.k ndio maana tunasoma yule mpanda farasi alikuwa amebeba mizani mkononi mwake hii inamaanisha kuwa ukitaka kitu lazima utoe kitu.
Kwa njia hii kanisa katoliki likiongozwa na utawala wa kipapa lilijikusanyia UTAJIRI MKUBWA SANA USIO WA KAWAIDA, sio ajabu hata leo hii tunaona jinsi taifa la Vatican lilivyo na utajiri mkubwa na halifanyi biashara yoyote ya kuliingizia kipato, linadhamini pesa za kujenga maseminari, na mashule, pamoja na miradi mingi mikubwa duniani kote inayogharimu mabilioni ya dola na bado halifanyi biashara yoyote. Utajiri huu ulianza katika kile kipindi mpanda farasi mweusi. Kwa kuwa hii dini ya uongo ilikuwa imeshaenea duniani kote, NURU ya Mungu ilififia sana, ikasababisha GIZA nene kulikumba dunia kwasababu hakuna mafundisho ya kweli yanayohubiriwa tena. Uchawi na ushirikina vilienea sana wakati huo.
Lakini pamoja na hayo Mungu aliachilia nguvu ya kulishinda hilo giza kwa watu wake wachache waliokuwa wanashikilia mafundisho ya mitume,na ile sauti iliyosikika ikisema usiyadhuru mafuta wala divai. Mafuta yanaashiria Roho Mtakatifu na divai inaashiria ufunuo wa neno la Mungu, hivyo basi lile kundi dogo la Mungu lililopitia kwenye hichi kipindi kirefu cha giza Bwana aliachia Roho ya ufunuo juu yao kwa mfano wa USO WA MWANADAMU ikiashiria hekima ya kibinadamu, ndipo kuanzia huo wakati Mungu akaanza kuwanyanyua wana-matengenezo kuirejesha ile Nuru ya Mungu iliyokuwa inakaribia kutoweka.
Hivyo basi Katika hichi kipindi cha giza hadi kwenye matengenezo ya kanisa, Mungu alinyanyua watu kama Martin Luther na fundisho la (mwenye haki wangu ataishi kwa imani) ambapo hapo mwanzo ilikuwa hairuhusiwi mtu yeyote kufundisha au kusoma biblia isipokuwa kwa viongozi tu wa kanisa katoliki!.hivyo Mungu aliendelea kunyanyua na wengine wengi kama, Zwingli, Calvin, Knox,Bucer, John Wesley na ujumbe wa (Pasipo utakatifu hakuna yoyote atakayemwona Mungu) n.k .Kwa ajili ya matengenezo ya kanisa na kulirejesha katika yale mafundisho ya mitume ya mwanzo ambayo shetani alijaribu kuyafukia.
Wakati huu wa FARASI MWEUSI, ulidumu katika makanisa matatu, yaani ; THIATIRA, SARDI, na FILADELFIA. Kuanzia mwaka AD 606-1520 AD.. ndipo ukaja wakati wa matengenezo ya kanisa.
MUHURI WA NNE:
Ufunuo 6:7-8 “Na alipoifungua muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu na yeye aliyempanda jina lake ni mauti, na kuzimu ikafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, na kwa hayawani wa nchi.”
Tunaona hapa yule MPANDA FARASI ambaye ndiye mpinga Kristo alipoanza kubadilika kutoka kwenye farasi mweupe akaenda kwenye farasi mwekundu, akaenda tena kuwa farasi mweusi na sasa kwa FARASI WA KIJIVUJIVU. Rangi ya kijivujivu inaashiria mchanganyiko wa rangi zote tatu yaani nyeupe, nyekundu na nyeusi. ambayo pia inaashiria udanganyifu na mauti.
Hii ni roho ya mpinga kristo inayotembea leo hii katika kanisa la mwisho la saba, (LAODIKIA), farasi huyu amechanganyikana na anazo tabia zote tatu za wale farasi wa kwanza. Ameitwa kuzimu na mauti inafuatana naye kwasababu katika kipindi cha mwisho anaonyesha rangi zake zote na kujifunua yeye ni nani kwa kuwaua watu na kuwapeleka kuzimu kwa namna mbili:
1) KWA KUWAUWA WATU KIROHO kwa mafundisho yake ya uongo, akiyaleta makanisa yote na dini zote pamoja (WORLD COUNCIL OF CHURCHES) Kwa ulaghai wake kama ilivyotabiriwa katika kitabu cha Daniel ili kuunda ile chapa ya mnyama, ambapo hakuna mtu atakayeweza kuuza wala kununua pasipo hiyo.
2) Na namna ya pili ni kwa kuwaua wakristo wote aidha kwa wazi au kwa siri wale wanaoenda kinyume na yeye, zaidi sana atakuja kuonyesha rangi yake katika kile kipindi cha ile dhiki kuu.
Kumbuka hazina yote ya dunia ipo Roma hii inaonyesha yule farasi mweusi anatembea katika utawala wa dini ya katoliki. Na tabia zote za wale farasi wa kwanza amezibeba huyu wa kijivujivu. unaweza ukaona tunaishi katika kipindi cha hatari kiasi gani.
Lakini pamoja na hayo Mungu ameachia nguvu ya kupambana na roho hii ya mpinga kristo nayo imefananishwa na yule MWENYE UHAI WA NNE, (Aliyefananishwa na TAI). Tai ana uwezo wa kuona vitu vya mbali sana na Bwana aliwafananisha manabii wake na Tai, hivyo basi katika kanisa hili la Laodikia ambalo ndio la mwisho Bwana ameachia Roho ya kinabii kuweza kuzitambua hila za yule adui, na kuturudishwa katika imani ya mababa(yaani mitume wa Kristo) na nguvu Mungu aliyoiachia ni ROHO YA UFUNUO ya kumtambua Mpinga Kristo na chapa yake na ujumbe wa kutoka kwake na kutokushiriki mafundisho yake ya uongo..
Ufunuo 18:4 Inasema “…tokeni kwake, enyi watu wangu msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.” Ikiwa wewe ni mkristo na hauna ndani yako Roho ya ufunuo ya kuona mbali kama Tai huwezi kamwe kumshinda shetani, utaangukia kumezwa na yule mnyama kwa mafundisho yake ya uwongo na unajua ni jambo gani linaambatana naye,
biblia inasema ni MAUTI NA KUZIMU, hakuna namna yoyote utakayoweza kumshinda shetani kama upo kwenye mifumo ya madhehebu na DINI ya uongo. umekwisha pokea chapa ya mnyama pasipo wewe kujijua, Kama hauna Roho Mtakatifu mwombe Mungu akupe na Roho ya ufunuo ya kulielewa neno lake.
Na huu wakati wa FARASI WA KIJIVUJIVU ulianza, mwaka 1906- Hadi mwisho wa dunia utakapofika pale utawala wa mpinga-kristo utakapohukumiwa na YESU KRISTO, BWANA WA MABWANA, na MFALME WA WAFALME.
MUHURI WA TANO:
Ufunuo 6:9-11 “Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vilevile kama wao.”
Hapa tunaona hakuna mwenye uhai yeyote akitangaza kufunguliwa kwa muhuri huu, hivyo hatuoni kanisa la mataifa likihusishwa wala mpanda farasi yoyote habari yao imeshakwisha.. lakini ulipofunguliwa muhuri wa tano zilionekana roho nyingi chini ya madhabahu zikimlilia Mungu. Sasa hizi ni roho za wayahudi waliouawa kipindi cha utawala wa kimabavu wa Adolf Hitler (Holocaust), watu hawa waliuliwa kwa sababu moja tu kuwa wao ni kwasababu wayahudi na si kingine!, historia inasema Hitler aliwaua wayahudi zaidi ya milioni 6 katika kipindi cha vita ya pili ya dunia.
Tunafahamu licha ya kwamba wayahudi wengi hawamwini YESU kuwa ni MASIA wao lakini bado ni watu wa Mungu na shetani anawachukia, kwasababu wanashika NENO la ushuhuda wao waliopewa na Mungu, (ambayo ni TORATI). Kwahiyo hapa tunaona kuwa hawa walikufa kwa ushuhuda wao, na sio ushuhuda wa Yesu Kristo, na pia hawa wanamwomba Mungu alipize kisasi juu ya maadui zao, kwani kulingana na torati kulipiza kisasi ni desturi ya wayahudi.
(Haya ni mateso ya wayahudi chini ya utawala wa dikteta Adolf Hitler)
kwamfano tunaona kuna maandiko yanayosema jino kwa jino, jicho kwa jicho,n.K ,Hivyo hatuwezi tukashangaa kwanini hapa walikuwa wanamwomba Mungu alipize kisasi juu ya maadui zao, lakini hiyo siyo desturi ya wakristo. Wakristo hawalaani wala hawaombi kisasi, bali wao husema baba uwasemehe, tunaona mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo na Stefano walivyofanya.Hivyo hizi roho zinazozungumziwa hapa ni wayahudi na sio wakristo.
Na pia tunaona walipewa nguo ndefu nyeupe, hizi zinaashiria kupewa neema ya wokovu kwa ushuhuda wao wenyewe walioushikilia, kwa lile agano Mungu alilomuahidia Ibrahimu na uzao wake,hawa ni wale wayahudi waliokuwa waaminifu na dini yao ya kiyahudi wakiishikilia torati kikamilifu hata kufa , wakaambiwa tena wangojee kwa kipindi kifupi mpaka idadi ya wajoli wao itimie ambao watakufa kama wao.hii inamaanisha katika kipindi cha ile DHIKI KUU ambayo mpinga kristo atawaua wayahudi wengi na kulivunja lile agano atakalofanya na wayahudi ambalo limezungumziwa katika kitabu cha Danieli sura ile ya tisa.
MUHURI WA SITA:
Ufunuo 6:12 “Nami nikaona, alipoifungua muhuri ya sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu,
13 na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi.
14 Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake.
15 Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima,
16 wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo.
17 Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?”
Hapa tunaona muhuri huu ulipofunguliwa dunia nzima iliathirika na ndiyo ile siku kuu ya kuogofya ya Bwana kama Yesu Kristo alivyoizungumzia katika katika mathayo 24:29-30 ” Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika; ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi”. Hii siku ya Bwana itakuja mwishoni mwa miaka mitatu na nusu baada ya kumalizika ile dhiki kuu.
Siku hii ya Bwana itadumu kwa kipindi cha siku 75 ikianzia kwa kumimina ghadhabu ya Mungu katika dunia, ambayo itahusisha vita vya harmagedoni (ufunuo 19-21, zekaria 14:1-4, 12).ndani ya siku hizi 75 kutakuwa pia na kufufuliwa kwa watakatifu waliouawa katika kipindi cha dhiki kuu (ufunuo 11:18, 20:4), itamalizia na hukumu ya mataifa (mathayo 25:31-46) kabla ya kuingia katika matengenezo ya utawala wa miaka 1000 wa Bwana Yesu Kristo (mathayo 19:28).
hizi siku 75 zinapatikana kutoka katika zile siku 1335 zilizozungumziwa katika kitabu cha daniel 12:12. siku hizi 1335 ukitoa siku 1260 (au miezi 42) ambayo mpinga kristo atatawala baada ya kuikomesha sadaka ya kuteketezwa ya daima daniel 9:24-27″……Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu.”
MUHURI WA SABA:
Ufunuo 8:1 “Hata alipoifungua muhuri ya saba, kukawa kimya mbinguni kama muda wa nusu saa. “
Mstari wa pili unaelezea juu ya wale malaika waliojiweka tayari kupiga baragumu ambayo ni habari nyingine isiyohusiana na muhuri wa saba, Huu ukimya mbinguni unaashiria kuna jambo linakwenda kutokea ambalo ndilo tunaloliona katika ufunuo sura ya kumi.
Kumbuka kulingana na mtiririko wa matukio yatakayotokea siku za mwisho, ni dhahiri kuwa Muhuri wa Saba utatimia kabla ya Muhuri wa sita kutimia.
katika sura ya kumi.
Ufunuo 10:1 “Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto.
2 Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi.
3 Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.
4 Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike”
Malaika huyu anayeonekana hapa si mwingine bali ni Bwana Yesu Kristo akiwa ameshika kile KITABU KIDOGO. kumbuka kitabu hichi ndio hicho kilichokuwa kumefungwa na mihuri 7, Na ndani ya muhuri huu wa saba ambao bado haujafunuliwa kwetu kwa sasa lakini utakapokuja kufunuliwa na upo mbioni kufunuliwa, UTAMPA BIBI ARUSI WA KRISTO IMANI YA KWENDA KWENYE UNYAKUO (ambapo ukisoma utaona siri hii imejificha katika zile ngurumo saba Yohana alizoambiwa asiziandike Ufunuo 10:4). Na muhuri huu wa saba utatimia kabla ya muhuri wa sita kutimia, kwasababu muhuri wa sita unaelezea siku kuu ya Bwana ambayo ni mwisho wa mambo yote.
kulingana na 1thesalonike 4:16-17 “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele”.
Kuja kwa Bwana kutafuata hatua tatu, ya kwanza ni Bwana atakuja na mwaliko (shout) na ya pili ni sauti ya Malaika Mkuu na ya tatu ni parapanda ya Mungu.
Hatua ya kwanza: ya mwaliko ndiyo tuliyopo sasa hivi iliyoletwa na Mjumbe wa kanisa la saba (William Branham) yenye ujumbe wa kutuandaa sisi kumpokea Kristo na kuturudisha katika ukristo wa biblia.
Mathayo 25:6 “Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki” Mjumbe wa kanisa la saba alikuja kututangazia ujio wa Bwana Yesu Kristo ambao ni wakati wa sisi kuzitengeneza taa zetu na kuwa tayari kumlaki Bwana Yesu mawinguni.
Hatua ya pili: ni sauti ya Malaika mkuu. na ndiye tunayemwona katika ufunuo 10 na si mwingine zaidi ya Yesu Kristo, na ujumbe wake utakuwa kwa yule bibi arusi aliyekwisha kujiweka tayari kumlaki, bikira safi ambaye taa yake inawakaa, huyu ni mkristo aliyebatizwa na Roho Mtakatifu aliyejitenga na uasherati wa yule kahaba (dini ya katoliki na madhehebu yote) yasiyofanya neno la Mungu kuwa mwongozo wao na kushikilia mafundisho ya wanadamu na ibada za kipagani. Huyu bibi arusi atakuwa bikira ndiye pekee atakayeisikia sauti ya malaika mkuu ambayo itahubiriwa na zile ngurumo saba tunazoziona katika kitabu cha ufunuo 10:3-4 Yohana alizoambiwa asiziandike lakini mwingine yoyote asiye bikira safi hatoweza kuisikia sauti ya hizo ngurumo saba.
NGURUMO SABA zitakuwa ni Sauti saba(watu,au huduma,) ambazo Mungu atazinyanyua katika kipindi hichi cha mwisho na kuleta uamsho mkuu duniani kote, ambazo kupitia hizi sauti saba tutapata imani itakayotuwezesha sisi kwenda katika unyakuo. Na hizi ngurumo saba zipo karibuni kutoa sauti zake..je? umejiweka tayari? unaye Roho Mtakatifu? kumbuka watakaoweza kuupokea ujumbe wa ngurumo saba ni bibi arusi tu mwenye Roho wa kristo. Na wakati huo ukifika kutakuwa hakuna muda tena, ni wakati wa wewe kutengeneza mambo yako sasa vizuri kwa Bwana.
Hatua ya tatu: na ya mwisho ni parapanda ya Mungu. katika kipindi hichi kila mmoja wetu aliye mkristo ataisikia sauti ya Mungu ikimwita na gafla tutaona mabadiliko ya miili yetu na kuchukuliwa juu mbinguni kwa Bwana milele na milele.
Kwahiyo kwa kuelewa Ufunuo wa MIHURI SABA, utaweza kufahamu kalenda ya Mungu na wakati unaoishi kwamba tunaishi katika siku za mwisho.
Mihuri saba (Ufunuo 6:1-17, 8:1-5 tarumbeta saba (Ufunuo 8:6-21, 11:15-19), na mabakuli saba (Ufunuo 16:1-21) ni msuluro wa aina tatu za hukumu nyakati za mwisho hukumu kutoka kwa Mungu. Hukumu itaendelea kuwa mbaya zaidi nay a kustaajabisha pakubwa huku nyakati za mwisho sikiendelea. Mihuri saba, tarumbeta, na bakuli ni kushikamana zimeunganishwa. Mhuri wa saba utakaribisha tarumbeta saba (Ufunuo 8:1-5), na baragumu ya saba itakaribisha bakuli saba (Ufunuo 11:15-19, 15:1-8).
za kwanza nne kati ya ile mihuri saba zinajulikana kama farasi wanne wa ufunuo. Muhuri wa kwanza unakaribisha Mpinga Kristo (Ufunuo 6:12). Mhuri wa pili husababisha vita vikubwa (Ufunuo 6:3-4). Tatu wa ile mihuri saba husababisha njaa (Ufunuo 6:5-6). Mhuri wa nne utaleta pigo la njaa zaidi, na vita zaidi (Ufunuo 6:7-8).
Mhuri wa tano inatuambia kuhusu wale ambao watakuwa mashahidi kwa ajili ya imani yao katika Kristo nyakati za mwisho (Ufunuo 6:9-11). Mungu anasikia kilio chao kwa ajili ya haki na kutoa katika muda wake katika mfano wa muhuri wa sita, pamoja na tarumbeta na bakuli ya hukumu. Wakati mhuri wa sita kati ya ile mihuri saba utatokea, tetemeko la ardhi hutokea, na kusababisha mageuzi mkubwa na ya kutisha na uharibifu -pamoja na matukio ya angani kawaida (Ufunuo 6:12-14). Wale ambao wanaishi wana haki ya kupiga kelele, "Tuangukieni, tusitirini mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi na hasira ya mwana kondoo. Kwa maana siku kuu, ya hasira yao, imekuja, na yeye ni nani awezaye kusimama?" (Ufunuo 6:16-17).
.
Tarumbeta saba zimeelezewa katika Ufunuo 8:6-21. Tarumbeta saba ni yale "yaliyomo" katika mhuri wa saba (Ufunuo 8:1-5). Baragumu ya kwanza husababisha mvua ya theluji na moto ambao utaiharibu mimea katika dunia (Ufunuo 8:7). Mbiu ya pili huleta kile kinaonekana kuwa mlima kupiga bahari na kusababisha kifo cha viumbe vya baharini (Ufunuo 8:8-9). Mbiu ya tatu ni sawa na ya pili, ila unaathiri maziwa duniani na mito badala ya bahari (Ufunuo 8:10-11).
Tarumbeta ya nne kati ya zile saba husababisha jua na mwezi kuwa giza (Ufunuo 8:12). Matokeo ya tarumbeta ya tano yatakuwa pigo la " kipepo la nzige" ambayo yatashambulia na kuwatesa wanadamu (Ufunuo 9:1- 11). Baragumu ya sita inatoa jeshi la mapepo ambayo itaua thuluthi moja ya binadamu (Ufunuo 9:12-21). Baragumu ya saba itaita malaika wa saba wenye mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya Mungu (Ufunuo 11:15-19, 15:1-8).
Hukumu ya bakuli ya saba imeelezewa katika Ufunuo 16:1-21. Hukumu ya bakuli la saba iliyoitwa na baragumu ya saba. Bakuli ya kwanza husababisha vidonda vyenye maumivu yatakayo wakumba wanadamu (Ufunuo 16:2). Matokeo ya bakuli la pili ni kifo cha kila kilicho hai katika bahari (Ufunuo 16:3). Bakuli la tatu husababisha mito kubadilika na kuwa damu (Ufunuo 16:4-7). La nne kati ya yale mabakuli saba litasababisha joto la jua litakalozidi na kusababisha maumivu makubwa (Ufunuo 16:8-9). Bakuli la tano litasababisha giza kubwa na kuongezeka kwa vidonda vya bakuli la kwanza (Ufunuo 16:10-11). Matokeo ya bakuli la sita ni katika mto wa Frati kuwa kavu na majeshi ya Mpinga Kristo waliokuwa wamekusanyika pamoja kupigana vita ya Amagedoni (Ufunuo 16:12-14). Matokeo ya bakuli la saba ni tetemeko la ardhi na kufuatiwa na mvua ya theluji kubwa (Ufunuo 16:15-21).
Ufunuo 16:5-7 yamtangaza Mungu, "Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi, kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe, nao wamestahili. Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Wbana Mungu Mwenyezi, na sa kweli na za haki, hukumu zako
This site was designed with Websites.co.in - Website Builder
We appreciate you contacting us. Our support will get back in touch with you soon!
Have a great day!
Please note that your query will be processed only if we find it relevant. Rest all requests will be ignored. If you need help with the website, please login to your dashboard and connect to support